Tuesday, August 14, 2012

Ally Rehmtullah kuzindua mitindo Sept.8


Mwanamitindo maarufu nchini Ally Rehmtullah ameandaa onyesho kubwa na la kipekee la mitindo litakalofanyika Septemba 8 kwenye hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam na kurushwa moja kwa moja bure na tovuti ya www.ar.co.tz.

Rehmtullah amesema dhumuni la kuandaa onyesho hilo ni kuonyesha aina mpya ya mitindo ya mavazi aliyobuni hivi karibuni na harakati zake za kuinua kiwango cha kazi za mitindo ndani ya nchi.

"Nimepania kupanua wigo wa taaluma ya mitindo na mavazi nchini ili kazi za wanamtindo na wabunifu wa mavazi wa Tanzania zipate kupenya kwenye soko la ndani na la Afrika Mashariki na Kati wakati tayari kuna soko la pamoja katika jumuiya ya Afrika Mashariki," alisema.

Rehmtullah alisema kwamba onyesho hilo litakuwa la kipekee kwa sababu mavazi na onyesho litapambwa na rangi nyeupe, ubunifu wa hali ya juu pamoja na muonekano mpya wa mavazi yaliyofanyiwa utafiti mkubwa ili kuendana na utamaduni wa Mwafrika.

Alisema onyesho hilo litapambwa na wasanii mbalimbali wa muziki na wacheza shoo kutoka sehemu mbalimbali nchini.

"Kazi za mitindo na mavazi ndio mkombozi wa kweli katika kupunguza tatizo la ajira nchini kwa sababu ni sekta inayokua kwa kasi kubwa na inatoa ajira kwa vijana wengi wa kike na kiume," aliongeza.

Onyesho hilo linategemewa kuhudhuriwa na watu zaidi ya 400 wakiwemo viongozi mbalimbali kama mawaziri, wabunge, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa mashirika mbalimbali.

Onyesho hilo litakuwa ni la mialiko maalum na limepewa jina la Ally Rehmtullah 2013 Collection.

Wadhamini wa onyesho hilo ni Mercedez Benz, Belvedere Vodka, DULUX, RAHA, HUGO DOMINGO,THE Tanzanite Experience, Shiva Images, Farm Plant, Creative Infinities, Out Door, Stanbic Bank, Phoenicia Properties, Dar es Salaam Serena Hotel, Missie Popular Blog, Mo Blog, Quality Furniture na Mx Carter.

No comments:

Post a Comment